
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Bw. Juma Hassan Reli ahakikishe anazuia utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje hadi sukari inayozalishwa na kiwanda cha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda iishe.
Amesema haiwezekani kiwanda hicho cha pekee kinachozalisha tani 6,000 za sukari kwa mwaka kikakosa wateja wakati mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumamosi, Januari 18, 2020) wakati apotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo katika eneo la Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘A’ mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema ni vizuri wizara ikahahakikisha sukari inayozalishwa na kiwanda hicho inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kununuliwa kwa sababu wanauhakika na ubora wake kwa kuwa wameshuhudia uzalishaji wake kuanzia hatua ya awali miwa ikiwa shambani.
“Wizara ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia uingizwaji wa sukari kutoka nje. Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hatuwezi kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia.”
Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya viwanda hivyo ni lazima viwanda vya ndani vikalindwa. “Viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika.”
Amesema kitendo cha wizara hiyo kushindwa kuratibu vizuri suala la uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi kutakwamisha uwekezaji jambo ambalo ni sawa na kuihujumu Serikali kwa kuwa itasababisha wananchi kupoteza ajira pamoja na Serikali kukosa mapato.
Waziri Mkuu amesema “haiwezekani sukari inayotengezwa na kiwanda hicho ambayo ubora wake umethibitishwa na Shirika la Viwango Zanzibar ikakosa soko hii haiwezekani tukashindwa kununua tani 6,000 huku mahitaji yetu ni tani 36,000.”
Amesema sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika pamoja na kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment