
Rais Museveni akanusha madai ya kwenye mtandao wa kijamii kuwa anaonekana amechoka na kusema kuwa ni kwa sababu amepunguza mwili
Mlo kamili wa mihogo, viazi ulaya na mboga za majani umeweza kumsaidia rais wa Uganda, Yoweri Museveni kupunguza kilo 30, aliiambia BBC.
"Nina afya njema siku zote lakini daktari aliona kuwa nnazidi uzito hivyo nikaamua kupunguza," bwana Museveni alisema.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 75 anasema kuwa alikuwa hajazingatia uzito wake ambao uliongezeka mpaka ukufikia kilo 106.
Alikanusha katika mitandao ya kijamii kuwa "anaonekana amechoka" anasema kuwa ni kwa sababu ya kupungua kwa mwili wake tu ndio maana anaonekana tofauti.
Mwezi uliopita katika blogu yake binafsi, rais Museveni alisema "niliruhusu kuongezeka mwili wangu kwa sababu madaktari walikuwa hawajafafanua vizuri madhara ya kutopambana na unene".
Aliongeza kusema kuwa uzito wake wa sasa ni kilo 76 ambao ni sawa na urefu wa futi 5(170 sentimita).
Ingawa bwana Museveni hakusema imemchukua muda gani kupunguza kilo 30.
"Huwa ninakula viazi kidogo kwa sababu sili kabisa vyakula vya ulaya au Asia. Huwa ninakula vyakula vyetu tu ama mihogo, ndizi, mtama na mboga zetu za majani,"bwana Museveni alimwambia mtangazaji wa BBC Newsday Alan Kasujja.
" Kwa kawaida huwa ninakula kidogo asubuhi, mchana sili chakula, huwa nnakunywa maji na kahawa bila sukari kwa sababu sukari ni mbaya sana kwa afya," alisema.
"Majira ya saa moja jioni huw aninakula viazi ulaya kwa sababu vina wanga kidogo na ninakula mbogamboga nyingi pia ili kulidanganya tumbo langu kuwa nimeweka kitu kumbe hamna kitu," aliongeza.
Bwana Museveni amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 na ana mpango wa kuwania tena muhula wa sita ifikapo mwaka 2021.
Mwanamuziki aliyeamua kuwa mwanasiasa Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 37, anapanga kuwania dhidi yake.
Wiki mbili zilizopita bwana Museveni alitembea kwa kilomita 195 (maili 121) katika mapori ya magharibi mwa Uganda ambako aliwahi kufanya safari za namna hiyo mnamo mwaka 1986 baada ya serikali ya Milton Obote kupinduliwa.
No comments:
Post a Comment