Sunday, 2 December 2018

Vyama vya wafanyakazi Vyadai maoni yao hayakuzingatiwa wakati wa utungaji wa kanuni za Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)

Vyama vya wafanyakazi vimedai maoni yao hayakuzingatiwa wakati wa utungaji wa kanuni za Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini mamlaka ya usimamizi wa mifuko hiyo (SSRA) imesema hakuna haja ya kuzibadilisha.

Hivi karibuni umeibuka mjadala kuhusu mafao baada ya kanuni hizo kuondoa mfumo wa zamani wa kulipa asilimia 50 ya mafao ya mkupuo na badala yake mstaafu kuruhusiwa kuchukua asilimia 25 kwa mkupuo na asilimia 75 igawanywe ili ilipwe kama pensheni kwa kila mwezi kwa kipindi chote cha maisha ya mstaafu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU), Dk Paul Loisulie amesema pendekezo lao la kuboresha kikokotoo ilikuwa ni 1/540, miaka 15.5 na asilimia 50 ya fao la mkupuo na asilimia 50 inayobaki iwe pensheni ya kila mwezi.

Alisema walitoa mapendekezo mengi kuliko vyama vyote vya wafanyakazi na walipendekeza kikokotoo kiwe ndani ya sheria badala ya kuwekwa kwenye kanuni.

“Uzuri wa sheria inajumuisha maoni ya watu wote tofauti na kanuni ambazo zinaundwa na waziri,” alisema Dk Loisulie.

Alisema SSRA inaweza kuratibu kazi ya kupokea maoni ya wadau wote kwa lengo la kurekebisha kikokotoo kilicholeta taharuki na hivyo kutuliza wafanyakazi.

“THTU itawakutanisha wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii ili kuandaa mapendekezo ya kina na kuyawasilisha SSRA na wizara husika kwa ajili ya mjadala na ufumbuzi,” alisema Dk Loisulie.

Naye rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamuhokya alisema walihangaika sana wakati kanuni hizo zikiundwa, lakini hawakufikia muafaka, na amewataka wanachama watulie kwanza.

“Vikao vya kisheria vitafanyika wiki ijayo, kelele ni nyingi kwa sasa wafanyakazi wanaona hatujatimiza wajibu wetu kwao,” alisema Nyamuhokya.

“Tuombe tu wawe na subira baada ya vikao hivyo, tutaeleza msimamo wetu.”

Alisema kabla ya kupitishwa kanuni hizo, mjadala baina yao na mamlaka husika ulichukua zaidi ya miezi mitatu na baada ya kikao cha wiki ijayo, wafanyakazi ambao ni wanachama wao wataelezwa hatua itakayofuata.

Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alisema utoaji wa mafao mkupuo wa asilimia 50 unahatarisha uhai wa mifuko husika na hata iliyokuwa inafanya hivyo, utafiti uliofanyika ulibaini haiwezi kuwa endelevu.

“Uundwaji wa mifuko iliyokuwa inatoa mafao mkupuo ilikuwa na makosa tangu awali. Mfano mfuko wa PSPF ulikuwa na mwenendo mbaya kama usingeunganishwa, ulikuwa unahitaji marekebisho makubwa,” alisema Isaka.

Alisema kwa sasa haoni haja ya kubadilishwa kwa kanuni zilizopitishwa za kikotoo wala sheria, badala yake mamlaka itaongeza nguvu katika kutoa elimu.

“Watu wakitaka mafao ya mkupuo yawe asilimia 50, haiwezekani na hiyo itakuwa sio pensheni tena, labda tuiite mfuko wa akiba,” alisema Isaka.

“Hata hivyo, wengi wanaolalamika ni wale wa NSSF ambao mabadiliko haya hayawahusu na wengine wanaoleta malalamiko hapa ofisini si wachangiaji wa mfuko wowote.”

No comments:

Post a Comment