Friday, 11 October 2019

Siasa za Tanzana: Kikwete dhidi ya viongozi wenye tabia za umwamba

Katika medani za siasa nchini Tanzania kuna neno jipya limeingia na kusambaa kama moto wa nyika, 'mwambafai'.
Neno hilo limetokana na hotuba ya hivi karibuni ya rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akijadili mada ya "Urithi wa Mwalimu Nyerere Katika Uongozi, Maadili, Umoja na Amani katika Ujenzi wa Taifa".
Tanzania inaelekea kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha aliyekuwa rais wa awamu ya kwanza, Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 jijini London, Uingereza.
Hotuba ya rais mstaafu Kikwete ni gumzo kwa kuwa amekemea mwenendo mbaya wa wanasiasa na viongozi kote nchini, na kuwakumbusha umuhimu wa kujali haki,utu, ukweli, kusikiliza mawazo kinzani, uongozi bora na demokrasia mambo ambayo yalisisitizwa na mwasisi wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere.

Je, Kikwete amesema nini hasa?

Akizungumza katika Kongamano la Miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dar es salaam, rais Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi alirusha kombora kwa viongozi wa sasa kuwa wanakosa sifa ambazo zilimfanya Mwalimu Nyerere akubalike, aheshimike na kupendwa ndani na nje ya nchi.
"Dhamana ya uongozi haikufanyi wewe uwe ni mtu zaidi ya raia wengine wowote waliopo pale. Haikufanyi wewe uwe na haki zaidi kuliko mtu mwingine ambaye si kiongozi. Anao wajibu wake wa uongozi kwako na wewe unao wajibu wako kwa kiongozi wako," alisema Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Kikwete aliongeza kwa kusema, "Na hili ni jambo kubwa kwa viongozi kutambua kwamba kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi. Kujimwambafai (kujifanya mwamba) hivi wala hakukufanyi uwe kiongozi zaidi. Una wakati wa kutekeleza majukumu yako lakini unapokuwa na binadamu wenzako ni wanadamu kama wewe."
Matukio ya wakuu wa mikoa na wilaya kuwasweka watu mbalimbali mahabusu yanashabihiana na ushauri uliotolewa na Kikwete wa uongozi wa kujimwabafai mwambafai.
Sheria ya Tawala za Mikoa No. 9 ya mwaka 1997 kwa wakuu wa Wilaya na wakuu wa Mikoa imekuwa ikitumiwa vibaya na viongozi wa ngazi hiyo kiasi kwamba malalamiko ya wananchi na wanaharakati za haki za binadamu yamekuwa makubwa.
Baadhi ya watu wamekuwa wakikamatwa kwa amri za Wakuu wa Wilaya kuwaweka ndani saa 48 kinyume na Katiba na misingi ya Haki za Binadamu.
Kumekuwa na malalamiko juu ya matumizi ya sheria hiyo ambayo wakuu hao wamekuwa wakiwaweka ndani wanasiasa na watu mbalimbali huku sababu za kufanya hivyo zikiwa hazieleweki.
Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere
Takwimu za Kituo cha Haki za Binadamu nchini (LHRC) zinaonyesha kuwa mnamo Julai 30, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexandar Mnyeti alitoa kauli ya kumkamata na kumweka ndani saa 48 Mwanasheria, Wakili Meinrad Menino D'Souza pamoja na mteja wake akiwa anatimiza majukumu yake ya kiwakili.
Agosti 16, 2018 Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya aliamuru kukamatwa kwa Wakili Edward John Mrosso ambaye baadae aliachiwa kwa dhamana akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mteja wake.
Amri zote hizo ni kinyume cha Tamko la Kimataifa kifungu cha 16 la Majukumu ya Mawakili 1990 na Kinyume na haki ya uwakilishi kama inavyotambuliwa na Sheria ya Mawakili Sura ya 341 ya mwaka 2002.
Agosti 15, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila aliamuru wanakijiji wa Kijiji cha Ngole wakamatwe na kuwekwa ndani kwa tuhuma za uharibifu wa miundo mbinu ya maji.
Kuamuru wanakikiji wote wakamatwe ni kinyume na haki ya asili pamoja na dhana ya kutokuwa na hatia kwa mujibu wa Ibara ya 13(6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, matumizi ya mabaya ya kifungu cha 7 na 15 cha Sheria ya Tawala za Mikoa, 1977 ni kinyume na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, Ibara ya 13(2).
Ushauri wa rais mstaafu Kikwete unagusa mwenendo huo, ambao hauna tofauti na kujimwambafai, sawa na kusema viongozi kuwa na matumizi makubwa ya nguvu na kuonyesha umwamba pamoja na vitisho dhidi ya wananchi au watu wenye mawazo tofauti na mamlaka zilizopo madarakani.

Je, nani anakubaliana na Kikwete?

Dkt. Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Jakaya Kikwete ni rais mstaafu na ana wajibu wa kuishauri serikali, chama na kuonya jamii katika mambo ya uongozi. Ametimiza wajibu wake na viongozi wa sasa wanapaswa kupokea ushauri hata kama ushauri huo unawaumiza.
Alipoulizwa kuhusu mapokeo ya ushauri wa Kikwete kwa pande zote mbili kwa maana ya chama tawala CCM na vyama vya upinzani, Dkt. Mbunda alisema, "zipo taarifa na dalili za wazi zinaonyesha ujumbe wa rais mstaafu Kikwete haujapokelewa vizuri, kwa pande zote mbili CCM na upinzani. Kikwete ni kiongozi wa kundi la wastaafu ambao wanashauri iwe viongozi na wananchi tunapenda au hatupendi. Kuna watu wanaopata hisia za kuumizwa na maneno hayo, lakini yote yanalenga kuijenga nchi. Huwezi kukataa ushauri wa Kikwete,"
Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) amesema kauli ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete inaonyesha yapo matendo ambayo hayakubaliki kiuongozi na hakubaliani nayo.
"Kikwete ni kama bosi mstaafu, bado anapata taarifa nyingi sana za ndani kabisa ya serikali na chama (CCM). Nafikiri wakubwa wa chama hawafurahishwi na mtindo wa uongozi wa sasa, tukikumbuka hivi karibuni Makatibu wakuu wastaafu walilalamikia kuvunjiwa heshima na mwanaharakati mmoja.
Anaongeza kuwa "Kuna manung'uniko ya suala la ubaguzi wa wazi unaofanywa sasa, hali ambayo vigogo wa chama inawakera. Mfano, tumeshuhudia hotuba za hivi karibuni (wilaya ya Tunduma mkoani Songwe) imejidhihirisha wazi wananchi wanaoishi kwenye majimbo yenye wabunge kutoka kambi ya upinzani wana wakati mgumu. Kikwete amefanya jambo sahihi kutumia jukwaa la Mwalimu Nyerere kusema aliyoyasema na nadhani itasaidia kuwarekebisha viongozi wa sasa ikiwa wataamua kujifunza."
Licha ya juhudi kubwa za serikali ya awamu ya tano inaendelea kujenga miradi mingi ya maendeleo, lakini inakabiliwa na changamoto ya kuondoa hofu miongoni mwa wananchi hususani wenye mitazamo kinzani au mawazo tofauti kama alivyosema rais mstaafu Kikwete kwenye kongamano tajwa.
Kumekuwa na wimbi la watu mbalimbali kukamatwa na kutupwa korokoroni kwa sababu za kuikosoa au kuandika maneno yasiyopendwa na serikali au viongozi wake kupitia mitandao ya kijamiii. Uhuru na ushindani wa mawazo ndiyo msingi wa kukua jamii yoyote.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kutambua hilo amewakilisha sauti ya watu wengi ambao wanaona kuwa uwanja wa uhuru wa mawazo kinzani ni kama vile unapigwa virungu.
Uhuru wa mawazo wa mtu anayesapoti serikali na yule ambaye anapingana nayo kimtazamo hauwezi kulingana. Ni muhimu kuikuza jamii kimawazo na kuwafanya watu wake washindane.
Kikwete amewakilisha sauti za wale wanaoamini kuwa kiongozi anapokosolewa haina maana ananyimwa hadhi ya uongozi bali ni mchakato wa kitaifa katika kujadili masuala yanayaowakugusa.
Ndiyo kusema wananchi wanayo haki ya kujali masuala yanayohusu nchi yao, hawana namna nyingine iwe yenye tija ama isiyo na tija, ilmradi wanafundishana namna masuala ya nchi yalivyo muhimu.
Uhuru walionao wanasiasa na wanachama wa CCM ni tofauti na ule wa vyama vya upinzani ambavyo si ajabu kusikia wanasiasa na wanachama wa CHADEMA,TLP,Chauma,Cuf,ACT-Wazalendo kwa kutaja vichache.
Mathalani CCM wanao uhuru wa kufanya mikutano na hamasa za 'CCM ya Kijani' mikoa na wilaya mbalimbali nchini, wakati vyama vya upinzani vimekuwa vikikutana na changamoto ya vibali na kunyimwa fursa hiyo.
Ushauri wa Kikwete unapata uungwaji mkono kutokana na mazingira yalivyo sasa katika nyanja ya siasa, ambapo kiwango cha ustahimilivu kimeshuka mno. Matamko ya kisiasa kutoka vyama vya upinzani au taasisi zake ambayo yanapaswa kujibiwa kisiasa na CCM, yamekuwa yakijibiwa na msemaji wa serikali, jambo ambalo linadhoofisha taasisi za chama tawala na kuwanyima wanasiasa uwanja wa kutamba pamoja na kufanya kazi zao.

No comments:

Post a Comment