
Viongozi wa ulimwengu wanakusanyika mjini Berlin leo Jumapili kujadili mpango mpya wa amani ya nchini Libya. Mkutano huo wa kilele unalenga kuumaliza mzozo katika nchi hiyo na kuiepusha kugeuka kuwa "Syria ya pili".
Wadau muhimu wanakutana Jumapili mjini Berlin kujadili makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Libya yanayoyumba. Wakati huo huo washiriki kwenye mkutano huo wanataka kutafuta njia ya kukabiliana na nchi za kigeni zinazoingilia kati masuala ya nchi hiyo inayokumbwa na machafuko tangu kuzuka ghasia za kuipinga serikali za mwaka 2011 zilizoungwa mkono na nchi wanachama wa jumuiya ya kijeshi NATO.
Ujerumani na Falme za Kiarabu (UAE) zimetoa wito wa pamoja kwa pande zote katika mzozo wa Libya kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano ya muda mrefu na kwa vikosi vya kigeni kuondoka nchini humo.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema wito huo ulitolewa baada ya kufanyika mkutano kati ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed al Nahyan, kabla ya mkutano wa kilele kuhusu amani ya Libya ambapo viongozi wa kimataifa wanakutana mjini Berlin mnamo Jumapili 19.
Viongozi hao wawili wamesisitiza kwamba mzozo wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi, bali kwa kudumisha amani na utulivu ambavyo vitafikiwa kwa njia ya mazungumzo. Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan amesema Falme za Kiarabu zingefanya kila jitihada kusaidia utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa Berlin kuhusu Libya.
UAE ni mmoja wa washirika muhimu zaidi wanaomuunga mkono kiongozi wa waasi jenerali Khalifa Haftar ambaye vikosi vyake vinadhibiti sehemu kubwa ya Libya na wanaipinga serikali ya Waziri Mkuu Fayez al-Serraj iliyopo katika mji mkuu wa Libya, Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment