Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akimkabidhi funguo za matrekta manne Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Dkt. Eligy Shirima (aliyekaa)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akimkabidhi funguo za matrekta matatu Meneja wa Shamba la Malisho Vikuge Bw. Richard Mdegipala
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na.
Edward Kondela
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara hiyo
ina mpango wa kuondokana na changamoto ya malisho ya mifugo ambayo imekuwa
ikisababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Prof. Gabriel amesema hayo katika
Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, kwenye hafla fupi ya kupokea matrekta saba kwa
ajili ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) pamoja na Shamba la Malisho
Vikuge kupitia mradi wa kuunganisha matrekta wa URSUS-TAMCO unaofadhiliwa na Serikali
ya Poland.
Akizungumza katika hafla hiyo
katibu mkuu huyo amesema matrekta manne ambayo yamenunuliwa na TALIRI kwa njia
ya mkopo wa miaka miwili wenye thamani ya takriban Tshs. Mil 220 na matrekta
matatu ambayo yamenunuliwa kwa fedha taslimu Tshs. Mil 192.1 na Ofisi ya
Msajili Hazina kwa ajili ya Shamba la Malisho Vikuge, yatatumika kwa ajili ya
kilimo kwenye mashamba ya malisho ya mifugo na kuongeza wingi wa upatikanaji wa
malisho na yenye ubora kwa mifugo pamoja na kuondoa migogoro ya wafugaji
kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima pamoja na ufugaji wa kuhamahama
kwa ajili ya kutafuta malisho.
“Wizarani tunataka kuondokana
na tatizo la malisho katika nchi hii ambalo limeainishwa kwenye ibara ya 25 katika
ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, changamoto ya malisho ni kubwa kwa
wafugaji tunaamini tutakapoondokana na changamoto ya malisho, changamoto ya
maji tutapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro iliyopo, tutapunguza tatizo la
ubora wa mifugo yetu, ndiyo maana tumeamua kuanzia Shamba la Malisho Vikuge.” Alisema
Prof. Gabriel
Katibu mkuu huyo pia ameitaka
TALIRI kuhakikisha matrekta hayo yanatumika ipasavyo kwa ajili ya kuzalisha kwa
kutumia mtaji huo na kulipa deni kwa wakati ili taasisi nyingine za serikali
zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ziweze kunufaika na mkopo huo ikiwemo
Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) ambayo imekuwa na mashamba makubwa ya
uzalishaji wa mifugo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Prof. Damian Gabagambi, shirika ambalo
linasimamia mradi wa kuunganisha matrekta wa URSUS-TAMCO amesema faida ambayo
wanataka kuiona kupitia mradi huo hapa nchini ni kubadilika kutoka kilimo cha
mkono hadi kilimo cha kutumia matrekta.
“Serikali ilipoanzisha mpango
huu haikuanzisha ili kupata faida kama wafanyabiashara wengine, faida ambayo serikali
inatarajia kupitia mpango huu ni kilimo kilichobadilika, kilimo ambacho
kinaondoa jembe la mkono kwa hiyo kupitia mradi huu, serikali imejipanga
kupeleka jembe la mkono makumbusho.” Alisema Prof. Gabagambi
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa TALIRI Dkt. Eligy Shirima na Meneja wa Shamba la Malisho Vikuge Bw.
Richard Mdegipala wamesema wanatakiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo
hususan kwa kuboresha malisho ya mifugo na kuondokana na tabia ambayo wafugaji
wengi wanatumia kwa miaka mingi ya kutafuta malisho ya mifugo yao porini.
Aidha wamesema matrekta hayo
yatatumika pia na majirani wa taasisi ya TALIRI pamoja na Shamba la Malisho
Vikuge na kwamba matrekta hayo yatawawezesha kuongeza gawio kwenye mfuko mkuu
wa serikali.
Hadi sasa Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) kupitia mradi wa kuunganisha matrekta wa URSUS-TAMCO
limeshauza matrekta 413 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwisho
|
No comments:
Post a Comment