Tuesday, 28 May 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU AAGIZA TAWA IUNDE TUME KUCHUNGUZA KIFUTA MACHOZI WILAYANI BUNDA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa wilayani Bunda mkoani Mara kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye ofisi za kijiji wakati wanyamapori wakali na waharibifu wanapoharibu mazao.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakimsikiliza Naibu Waziri waMaliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati wa mkutanao wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya ,msingi ya Sarakwa mara baada ya kusikiliza malalamiko yao kuhusu malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akisalimiana na baadhi ya watumishi wa wilaya ya Bunda mkoani Mara mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa ajili ya kikazi ya siku moja
 Mbunge wa jimbo la Bunda vijijini, Boniface Getere  akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwenye ofisi za kijiji wakati wanyamapori wakali na waharibifu wanapoharibu mazao yao
 Mwenyekiti wa kijiji cha Sarakwa, Samson Kapeta akizungumza na wananchi wake kabla ya kumkaribisha na Mbunge wa jimbo la Bunda vijijini, Boniface Getere  kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakiwa katika mkutano wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wilayani Bunda mkoani Mara
                                                               xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya  Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iunde timu ya kuchunguza uhalali wa malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kilichotolewa kwa wananchi  walioathiriwa   na wanyamapori wakali na waharibifu wa mazao katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Kanyasu ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea malalamiko na madai kutoka kwa baadhi ya wananchi wa vijiji 4 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wilayani Bunda mkoani Mara ambao  mazao yao yaliliwa na kuharibiwa na wanyamapori wakali wamekuwa hawalipwi  huku    wasiostahili ndo wamekuwa wanalipwa .
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Sarakwa, Mariwanda ,Unyali na Kihomboi vinavyopakana na  Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bunda mkoani Mara, Mhe.  Kanyasu amesema  kuwa mara  baada ya uchunguzi kukamilika wale watakaobainika kupokea fidia hiyo wale wasiostahili watachukuliwa  hatua kali za kisheria ikiwemo kuzirudisha fedha hizo.

‘’Nataka niwambie, wale waliopokea kifuta jasho na kifuta machozi kutoka serikalini wakati hawastahili lazima hizo fedha wazitapike” Amesisitiza Mhe. Kanyasu
Aidha, Mhe. Kanyasu amesema licha ya fidia hiyo kuendelea  kulalamikiwa kuwa kidogo ikilinganishwa na hali halisi ya maisha ya sasa,  wananchi ambao  mazao yao  yameharibiwa wanatakiwa kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria  iliyopo na sio vinginevyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Kanyasu amewataka wananchi wanaoharibiwa mazao yao na wanyamapori wakali na waharibifu  wakiwemo  tembo watoe taarifa ndani ya muda wa siku tatu  katika ofisi za vijiji katika maeneo yao  ili hatua za malipo ziweze kufanyika kwa muda.
Pia, Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa Serikali imeanza kupitia upya utaratibu wa kifuta jasho na kifuta machozi ili kiweze kuendana na gharama za maisha ya sasa.
Kwa upande wake Bw. Abel Hadawi, mmoja wa wananchi  ambaye mazao yake zaidi ya ekari 20 yaliharibiwa mwaka jana, amemweleza Naibu Waziri huyo  kuwa  amaekuwa akijaza fomu kwa ajili ya kulipwa fidia lakini kila malipo yanapokuja jina lake limekuwa halimo.
Kwa upande wake,  Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) kanda ya Ziwa, Emmanuel Nkya amewaeleza wananchi hao kuwa wanachotakiwa kufanya ni  kujaza fomu nne ili kuwe na nakala kuanzia ofisi ya kijiji hadi makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Naye Mbunge wa Bunda vijijini, Boniface Getere amemwomba  Naibu Waziri Kanyasu kuyashughulikia malalamiko ya wananchi wote wanaostahili kulipwa kifuta jasho na kifuta machozi kwa kuwa wengi wao wameathiriwa na kubaki omba omba kufuatia mazao yao kuharibiwa.

No comments:

Post a Comment