Baadhi ya wadau wa Maendeleo ya Mtoto nchini
wakifuatilia mada na mijadala mbalimbali wakati wa Mkutano wa kitaifa wa
wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto unaofanyika jijini
Dodoma kwa siku mbili.(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano WAMJW)
NA MWANDISHI WETU DODOMA
TAKWIMU za Hali ya Watu na Afya (TDHS 2015/2016)
zinaonyesha kuwa kuna tatizo kubwa kwenye lishe ya watoto wa umri chini
ya miaka 5 nchini ambapo imesababisha udumavu kwa asilimia 34 inayosababishwa
na uelewa mdogo wa wazazi kuhusu kunyonyesha watoto katika muda uliopendekezwa
ambapo asilimia 59 tu ya wakinamama ndiyo wanaonyonyesha watoto wao kama
inavyotakiwa na asilimia 51 ya akinamama wajawazito ndiyo wanaohudhuria
kliniki. Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mwakilishi wa
Katibu Mkuu Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Patrick Golwike
wakati akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt. John Jingu wakati wa
ufunguzi wa Mkutano wa kitaifa wa wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya
awali ya mtoto.
Bw. Golwike amesema kuwa Serikali imechukua
hatua mbalimbali katika kuboresha utoaji wa huduma za malezi, makuzi na
maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuandaliwa kwa
Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008) ambayo imeelekeza utoaji wa elimu ya malezi
na makuzi kwa jamii, Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) inayoelekeza
kuondoa vikwazo vyote vinavyomnyima mtoto haki kupata elimu na Sera ya
Afya(2006) inayoelekeza utoaji wa huduma bure za afya kwa watoto walio chini ya
maiaka 5 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 inayoelekeza masharti ya
usajili wa vituo vya kulelea watoto mchana na jinsi ya kuviendesha pamoja na
Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 ambapo inatoa
adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa yeyote atakayesababisha mtoto kukatisha
masomo.
Amesisitiza kuwa Serikali
imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja kutoka vifo
99 mwaka 2011 hadi vifo 43 mwaka 2016 kwa watoto 1,000 na katika kipindi
kama hicho, vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoka vifo 147 hadi
vifo 67. Mafanikio haya yanatokana na maboresho yaliyofanyika katika
utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2000.
Aidha, katika kuhakikisha
kuwa watoto wote wanapata haki ya kuendelezwa kielimu, na kulindwa
Serikali imehakikisha watoto wote nchini wanapata elimu bila malipo kuanzia
elimu ya awali hadi kidato cha nne na imeanzisha Kamati za Ulinzi wa wanawake na
watoto ambao ndio wasimamizi wakuu wa usalama wa Wanawake na Watoto na
zinaratibu vitendo vyote vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kuanzia
ngazi ya Taifa, Tawala za Mikoa hadi Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameongeza kuwa mpaka sasa
Serikali imeanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika mikoa 26 na
Halmashauri 89 kwa lengo la kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na Watoto bado
kunahitaji msukumo zaidi ili kufikia Halmashauri zote 185 na kujenga uwezo wa
Kamati hizi ili kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Nachukua fursa hii kuwashukuru
wadau wote mliochangia kwa hali na mali kufanikisha kufanyika kwa mkutano
huu na kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru sana Shirika la Children In
Crossfire kwa kushirikiana na Mtandao wa Malezi na Makuzi (TECDEN) kwa wazo
hili liliopelekea kuandaliwa kwa mkutano huu muhimu sana kwa maendeleo ya
watoto wetu” alisisitiza Bw. Golwike
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi (TECDEN) Bw. Bruno Ghupi ameishukuru
kwa ushirikiano baina ya wadau wa Maendeleo ya mtoto na Serikali katika
kuhakikisha mtoto anapata malezi na makuzi bora katika ukuaji wao ili kuwezesha
kuwa na watoto wenye afya bora na utimamu wa akili.
Wadau mbalimbali wa
Maendeleo ya Mtoto wanakutana Mkoani Dodoma kujadiliana kuhusu namna bora
ya kuwezesha malezi, makuzi na maendeleo ya Mtoto katika Mkutano wa kitaifa wa wadau wa malezi,
makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto unaofanyika jijini Dodoma kwa siku
mbili kuanzia tarehe 3 – 4 Desemba, 2018.
No comments:
Post a Comment