Friday, 7 February 2020

Majaliwa, Mbowe wavutana mikutano ya hadhara, tume huru ya uchaguzi

HOJA ya tume huru ya uchaguzi na kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara imeibuka bungeni, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema tume ni huru wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akisema majibu hayo ni mepesi.
Mjadala huo uliibuka jana bungeni wakati Mbowe alipouliza swali wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Hoja ya tume huru ya uchaguzi imeibuka siku za hivi karibuni na juma lililopita ilichagizwa na Ubalozi wa Marekani nchini, ambao ulimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa ahadi aliyoitoa kwa mabalozi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani, huru na haki huku ukisema unatarajia pia kutaundwa tume huru ya uchaguzi.
Jana katika swali lake, Mbowe alihoji ni lini Serikali itaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu, huku pia akitaka kujua mpango wa Serikali kuhakikisha kunakuwa na tume huru ya uchaguzi.
 “Ni miaka minne sasa tangu Serikali yenu imeweka zuio kwa vyama vya siasa kufanya wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya nchi na tunavyozungumza leo (jana) ni siku 262 zimebaki kufika Oktoba 25, siku ambayo nchi yetu ifafanya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
“Kwa busara zako binafsi katika Serikali ambayo wewe ni kiongozi mwandamizi, unafikiri ni lini mtaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi kujiandaa na Uchaguzi Mkuu?” aliuliza Mbowe.

No comments:

Post a Comment