Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu ameeleza kuwa, Wanasheria wa Wizara ya Nishati, Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wataanza kupitia
mikataba ya wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini ili kuchukua hatua za
kuwawajibisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa kusuasua.
Aliyasema hayo jijini
Dodoma wakati wa kikao chake na Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa, Wilaya na
wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, REA
na TANESCO.
“ Yako baadhi ya
maeneo ambayo Wakandarasi hawafanyi vizuri kama vile Mtwara, Arusha,
Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Shinyanga, Singida, Tabora (Kaliua, Uyui,
Urambo), Dodoma na Tanga (Wilaya ya Korogwe, Mkinga na Pangani), ambao
utekelezaji wao katika mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa
kwanza, wako chini ya asilimia 20,” alisema Mgalu.
Naibu Waziri alitoa
agizo kuwa, wakandarasi katika maeneo hayo wahakikishe kuwa, wanafanya kazi kwa
kasi na ufanisi ikiwemo kuweka magenge mengi ya kazi, uwepo vifaa na wasimamizi
wa miradi wa kutosha ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na Serikali na
pia kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kusambaza umeme vijijini.
Kuhusu hali ya
usambazaji umeme vijijini, Mgalu alisema kuwa, kuanzia Januari mwaka 2017 hadi
sasa jumla ya vijiji 1,098 vimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji
umeme wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Mradi wa Makambako-Songea, Mradi wa
Backbone na miradi ya umeme iliyo nje ya gridi.
Hivyo kwa ujumla alisema
kuwa, hadi sasa jumla ya vijiji 5,493 vimesambaziwa umeme nchini na vijiji
vilivyosalia ni 6,775 ambavyo vinaendelea kusambaziwa umeme kupitia REA III
mzunguko wa kwanza na wa pili.
Aidha, Naibu Waziri
wa Nishati, aliwakumbusha wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa miradi husika
inaleta tija kwa jamii kwa kuunganisha nishati hiyo katika sehemu mbalimbali
zinazotoa huduma za kijamii kama vituo vya afya na katika shughuli zinazokuza
uchumi wa wananchi kama vile mashine za kusaga na kukoboa nafaka au sehemu za
biashara.
Vilevile, Naibu
Waziri wa Nishati aliwakumbusha wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kuhusu kutekeleza agizo la
Serikali la kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila Wiki na kununua vifaa vya umeme
vinavyozalishwa hapa nchini.
Hata hivyo, alisema
kuwa viwanda vinavyozalisha vifaa hivyo chini ya ubora unaotakiwa vitaanza
kuchukuliwa hatua kwani vinachelewesha kazi ya usambazaji umeme nchini.
Kwa upande wake,
Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati katika kikao hicho, Haji
Janabi alitoa pongezi kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Naibu
Waziri wa Nishati kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme na kuwa na ari ya
kufanya kazi, usiku na mchana.
Aidha alitoa wito kwa
watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi kufanya kazi kwa bidii kama ilivyo
kwa viongozi hao wa Wizara na kuwa wabunifu. Alisema kuwa, baada ya kikao kazi hicho, Wizara na Taasisi
zitatekeleza ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri na kusimamia miradi
ya usambazaji umeme vijijini.
Kikao hicho
kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma,
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
REA, Mhandisi Amos Maganga.
Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu (katikati), akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu,
Wizara ya Nishati, Haji Janabi wakati wa kikao kazi na watendaji wa REA na
TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA,
TANESCO na Wizara ya Nishati. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa
Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa
TANESCO, Dkt Tito Mwinuka (wa pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA,
Mhandisi Amos Maganga (wa kwanza kulia).Baadhi ya watendaji wa REA na TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA, TANESCO na Wizara ya Nishati wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment