Tuesday, 11 December 2018

WALIOKIUKA MASHARTI YA NARCO MKATA WAPEWA MWEZI MMOJA KUONDOKA

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyekaa), akitoa maelezo kwa baadhi ya viongozi wa wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro juu ya kuwaondoa watu wasiotakiwa katika ranchi ya NARCO Mkata.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza katika mkutano wa hadhara na baadhi ya wafugaji katika Kata ya Parakuyo, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
……………………………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa ya Kilosa Mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Meneja wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuwaondoa wakulima wanaolima ndani ya ranchi hiyo ya Mkata, ambao walipewa vitalu na bila kuviendeleza, wanaokodishia vitalu wakulima na wasiolipa kodi za Serikali. 
Mhe. Ulega ameyasema hayo Jumtatatu hii (11.12.2018) alipokuwa ranchi ya NARCO Mkata wilaya ya Kilosa katika ziara yake ya kushughulia migogoro na malalamiko mbalimbali ya wafugaji katika mkoa wa Morogoro.
“Nawapa mwezi mmoja kuwaondoa wakulima wote ambao wanalima ndani ya ranchi NARCO Mkata, wale waliopewa vitalu wakashindwa kuviendeleza pamoja na ambao hawajalipa serikali kodi na wao waondolewe kwa mujibu wa Sheria na taratibu.” alisema Mhe. Ulega
Katika ziara hiyo wilayani Kilosa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefanya mkutano wa hadhara na wafugaji katika Kata ya Parakuyo kijiji cha Parakuyo na kuwaeleza wafugaji hao juu ya maagizi aliyotia kwa viongozi  wa wilaya hiyo kuhusu ranchi ya NARCO Mkata.
“Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na rais wetu anawapenda sana wafugaji na watu wote anatupenda, na alishatupa maagizo wizara kuwaondoa watu waliohodhi maeneo ya ranchi na kuwapa wafugaji wetu” alisema Mhe. Ulega
Aidha, akijibu hoja ya wafugaji kukosa elimu ya ufugaji wa kisasa wenye tija ikiambatana na elimu ya uzalishaji wa malisho, Mhe. Ulega aliwaagiza wataalam wa mifugo kutoka Wakala wa Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Mifugo (LITA) kupeleka wanafunzi kujifunza kwa vitendo katika kata ya Parakuyo na maeneo mengine ya wafugaji ili waweze kusambaza elimu kwa wafugaji.
Alifafanua pia hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina atazindua kampeni ya uogeshaji mifugo ambayo itafanyika mkoani Geita wilaya ya Chato ambapo kuogesha mifugo sasa itakuwa lazima.
Katika kampeni hii wizara inatoa bure dawa kwa ajili ya kuogeshea mifugo na tayari zimesambazwa katika mikoa yenye mifugo. Alifafanua dawa zilizotolewa zitaogeshea mifugo bure kote nchini na baada ya hapo itabidi mfugaji kulipia dawa kuogesha mifugo kila mara apelekapo mifugo yake kwenye josho.
Wafugaji hao walishukuru kwa kutembelewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, na kusema ujio wake umeleta matumaini makubwa katika kumalizika kwa changamoto zinazowakabili.
Aidha, wafugaji walimpongeza na kumshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali na kuwatetea wanyonge pia kwa mradi wa reli ya kisasa “Standard Gauge” ambao umewapa ajira vijana wao na pia utasaidia katika usafirishaji wa mifugo yao kwenda katika masoko ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment