Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mjini
Unguja na kumweleza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inahakikisha miradi inayohusu wavuvi inawanufaisha moja kwa moja.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia
yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Makame Ali Ussi, Naibu Katibu Mkuu
wa wizara hiyo Bw. Islam Seif Salum pamoja na watendaji wengine wizara,
Mhe. Ulega amesema lengo kuu la ziara yake ya siku moja kisiwani
Zanzibar ni kutazama shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu
Zanzibar kupitia mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari
ya Hindi (SWIOFISH).
“Tunahitaji tuone rasilimali
za bahari zinatunufaisha, mchango wake bado ni mdogo sana mradi wa
SWIOFISH una pesa nyingi lakini bado hatujaona mafanikio ya moja kwa
moja kuwasaidia wananchi tulikubaliana kuna mambo ya kurekebisha.” Alisema Mhe. Ulega
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid
Ali Juma amesema uchafuzi wa bahari, uwepo wa maharamia na uvuvi haramu
ni mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kukabiliana
nayo ili kuhifadhi bahari na kufanya sekta ya uvuvi kuwa yenye tija kwa
wananchi.
Mhe. Juma pia amesema Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika masuala yanayohusu uvuvi ili kubadilishana
uzoefu hasa baada ya hivi karibuni kuhudhuria mkutano wa “Blue Economy”
nchini Kenya ambapo nchi washiriki wa mkutano huo walikubaliana
kusimamia mambo mbalimbali ili kulinda rasilimali za Bahari ya Hindi.
Mara baada ya mazungumzo hayo,
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipata fursa ya
kukutana na watendaji wa wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa
Serikali ya Mapinduzi pamoja na watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Bahari Kuu Zanzibar ambapo amewataka kujenga mazingira ambayo
yatawanufaisha wavuvi hususan kwa kubuni teknolojia za kisasa kwa ajili
ya shughuli za uvuvi.
“Unajua viongozi wetu wanataka
kuona tunakuja na vitu gani vipya, mapinduzi gani mapya, tusikae na
sisi tukaendelea kufanya vile vile kwa maana shughuli za uvuvi za
kurithishana, jukumu letu viongozi ni kuwasaidia wavuvi hawa kupata
teknolojia ili kuwarahisishia shughuli zao badala ya sasa wakiendelea
kuvua kwa kubahatisha.” Alisema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega ametoa wito kwa
watendaji hao kutumia vizuri fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia
Shilingi Bilioni Tano kwa ajili ya mradi wa SWIOFISH ili kuleta
mapinduzi ya kweli katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha wanafanyakazi
kwa kasi kulingana na matarajio ya serikali zote mbili kwa wananchi
wake.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara hiyo kwa kutembelea na kujionea
namna teknolojia mbalimbali zinazotumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa
Bahari Kuu Zanzibar katika uhifadhi wa Bahari ya Hindi pamoja na kupata
taarifa sahihi za shughuli za uvuvi zinazofanywa baharini katika eneo la
Tanzania.

No comments:
Post a Comment