WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe jana alifika mbele ya Kamati
ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma na kuhojiwa kwa saa tano.
Membe aliyepata kugombea urais ndani ya chama hicho na kuingia tano bora katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alifika ofisi ya makao makuu ya CCM jana saa 3:10 asubuhi na kutoka saa 8:43 mchana.
Desemba 13 mwaka jana, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliketi na kuagiza makada watatu wa chama hicho waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya chama hicho baada ya kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali.
Makada hao mbali na Membe, ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba ambao nao watahojiwa.
Jana, akiwa ndani ya gari lake aina ya Range Rover Vogue baada ya kuhojiwa, Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa safari yake ya kuhojiwa na kamati hiyo ya maadili ilikuwa na manufaa makubwa kwake, kwa CCM na kwa taifa.
Mbunge huyo wa zamani wa Mtama, alisema amekuwa mtu mwenye furaha mara baada ya kuhojiwa, na anakwenda kula chakula kizuri yeye na mke wake hoteli ambayo haijulikani na kwamba mengine yatakuwa yakipatikana kidogo kidogo mara baada ya kushiba.
“Lakini niwaambie safari hii ya kuja Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana sana sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu, mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba.
“Kwa hiyo sasa hivi mimi na mke wangu tunaenda kula chakula kitamu sana kwenye hoteli moja ambayo haijulikani, ‘and then’ baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam,” alisema Membe.
Vilevile alisema amekuwa ni mtu mwenye furaha kwa sababu amepata nafasi ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa na pia amepata nafasi ya kufafanua mambo pamoja na kutoa mawazo yake.
“Nasema hivi, tulikuwa na mkutano wa masaa matano ya mijadala mizuri mikubwa ya kitaifa inayohusu chama chetu CCM, inayohusu nchi yetu na nimekuwa mtu wa furaha kubwa ajabu, kwa sababu nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa.
“Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu walitaka kuyajua, nimepata nafasi nzuri ya kutoa mawazo ya yale mambo ambayo niliombwa kutoa mawazo,” alisema Membe.
No comments:
Post a Comment