Majaliwa atoa maagizo mapya kwa Tanroads

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara
nchini (Tanroads) kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake kufanya
ukaguzi wa kina wa barabara na madaraja katika maeneo yao mara kwa mara.
Majaliwa aliyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua hatua za
ujenzi wa barabara ya mchepuo aliyoagiza ijengwe na Tanroads Machi 4 ili
kuondoa msongamano wa magari yaliyokwama kwa siku tano katika barabara
ya Dodoma-Morogoro.
“Nimepita mara ya pili kukagua hatua za ujenzi na nimeridhika kuona
maendeleo yake, barabara hii ya mchepuo imeondoa foleni iliyokuwepo,”
alisema Majaliwa.
Aliwasihi mameneja wa Tanroads kuhakikisha wanakagua vipenyo vya
madaraja yote, hususani ya muda mrefu kuona kama ukubwa wake unaruhusu
maji kupenya kwa urahisi, hasa vipindi hivi vya mvua nyingi.
Aliitaka Wizara na Tanroads kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa
matengenezo zinatumika kikamilifu ili kuboresha mawasiliano katika
barabara kuu na kuhakikisha zinapitika majira yote ya mwaka.
Alitoa wito kwa wananchi wote kuwa wavumilivu katika maeneo
yaliyopata athari za mvua, hasa katika barabara na madaraja wakati
Serikali inafanya utaratibu wa ukarabati wa miundombinu.
“Tunaelewa mvua zinanyesha, hivyo nawaasa Watanzania kuwa watulivu
wakati kazi ya ukarabati zinafanyika kwa dharura kwanza hadi hapo hizi
mvua zitakapoisha,” alisema Majaliwa.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kalavati la zege katika eneo la
Kiyegeya, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa
awali waliweka makalavati ya chuma yenye urefu wa mita 12 kila moja kwa
dharura ambayo yaliwezesha magari kupita njia moja.
Mfugale alisema kazi inayoendelea sasa ni ya kujenga kitako na
kuunganishwa na kalavati la awali ili kuwezesha magari mawili kupita kwa
pamoja.
“Hivi sasa magari yanayotoka njia ya Morogoro yanapita katika njia ya
awali na yanayotoka Dodoma yanapita njia ya mchepuo ili kuruhusu ujenzi
kuendelea,” alisema Mfugale.
Alisema kazi hiyo ya ujenzi inatarajia kumalizika baada ya wiki mbili
ili magari yaweze kutumia njia ya awali wakati wanaendelea na ujenzi wa
tabaka la lami.
No comments:
Post a Comment