Kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inanunua korosho yote ya wakulima inatimia kabla ya kipindi cha masika hakijashika kasi, uongozi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji umewatoa hofu wakulima wote wa mikoa ya kusini kuwa serikali inao uwezo wa kununua na kihifadhi korosho yote itakayonunuliwa.
Hakikisho hilo limetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Joseph Buchwaishaija wakati anahitimisha siku ya kwanza ya oparehseni ya ukaguzi wa maghala kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Ziara ya ukaguzi wa maghala inatokana maagizo ya kikao cha tathmini ya Operesheni Korosho kilichoitishwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga, ambapo pamoja na mambo mengine kilibaini ufinyu wa maeneo ya kuhifadhia korosho kutoka kwa wakulima” anasema Prof. Buchweishaija.
Kwenye ziara hiyo Prof. Buchwaishaija pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Viwanda) Ludovick Nduhiye na maafisa wengine waandamizi wa wizara hiyo walifanikiwa kukagua maghala ya korosho kwenye wilaya za Mtwara, Mtama, Masasi na Nachingwea na kubaini kuwa maghala makuu na yale ya uhifadhi yana nafasi ya ziada kuhifadhi korosho zaidi ya tani elfu arobaini na nane.
“Nachukua nafasi hii kuwatoa wasiwasi wakulima wote kwamba, maghala na sehemu za kuhifadhi korosho zetu sio tatizo tena, na tutahakikisha korosho zote ziliyopo kwenye AMCOS (vyama vya msingi) tunazisafirisha haraka iwezekanavyo kabla ya msimu wa mvua kuanza.” Anasisitiza Prof. Buchwaishaija.
Mbali na kukagua maghala ya kuhifadhi korosho, ziara hiyo pia ilikuwa na lengo la kukutana na makumpuni ya kubangua korosho ambayo yameonyesha nia na utayari wakati serikali itakapoanza kubangua korosho ilizozinunua moja kwa moja kutoka kwa wakulima.
Operesheni ya ukaguzi wa maghala mikoa ya kusni inatarajiwa kuendelea kwenye wilaya za mkoa wa Ruvuma kesho.
No comments:
Post a Comment